CHAMA cha ACTWazalendo kimejibu mapigo ya kauli zilizotolewa na Msemaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Christopher ole Sendeka, huku kikieleza kuwa kinakaribisha uchunguzi juu ya mali na madeni za Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Kabwe Zitto.
Aidha, chama hicho kimeeleza kuwa kitafurahishwa zaidi kama uchunguzi huo, utahusisha akaunti zake za benki na mfumo wa maisha yake binafsi.
Tamko hilo lilitolewa na Katibu wa Bunge na Serikali za Mitaa wa chama hicho, Habibu Mchange wakati akizungumza na wanahabari katika Makao Makuu ya ofisi za chama hicho zilizopo Kijitonyama Dar es Salaam jana. Mchange alisema wameshtushwa na kusikitishwa na tuhuma zilizotolewa na Sendeka ambazo hazina ukweli wowote.
“Tunavitaka vyombo vya uchunguzi vianze kazi hiyo mara moja, kwani tunaamini kuwa kama kuna kiongozi ambaye mali, madeni, maslahi na akaunti zake ziko wazi basi ni ndugu Zitto,” alisema Mchange.
Alisema kuwa Katiba na Kanuni za chama hicho huwataka viongozi wote wa chama kuweka hadharani tamko la mali zao na madeni, na kwamba Zitto alitekeleza matakwa hayo ya kisheria na mali pamoja na madeni yake yako hadharani katika mitandao ya kijamii.
Akizungumzia kuhusu Sendeka kutaka uchunguzi dhidi ya wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge ambao walikuwa wakisimamia mashirika ambayo yanatajwa kufanya vibaya ikiwemo Shirika la Hifadhi ya Jamii la NSSF na kumtaja Zitto, Mchange alisema, Sendeka pamoja chama chake ni kama wanaweweseka.
Alisema chama hicho kina taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambayo alitoa hati safi kwa Shirika la NSSF kwa hesabu za mwaka 2014/2015, ambayo ilimaanisha hakuona ufisadi wa aina yoyote.
Mchange alihoji ni taarifa ipi ya CAG ambayo Sendeka anaitumia na kuwa NSSF ilinunua ardhi kwa bei ya Sh milioni 800, iliyomhusisha kiongozi huyo wa chama hicho.
Alisema wanamtaka Sendeka kuacha kutoa tuhuma na badala yake ajikite katika kukishauri chama chake kutekeleza ahadi zake kwa wananchi. Pia chama hicho kitaendelea kuisimamia serikali katika mambo mbalimbali bungeni kama anavyofanya kiongozi wao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni