Tuesday, June 12, 2012
NENO LA KUTIA NGUVU ASUBUHI YA LEO: KASIMAME IMARA !!!
Inawezekana dunia imekupiga dafrau mpaka umefikia kuona kuwa maisha yako haya maana yo yote hapa duniani.
Inawezekana jamii imekuaminisha kuwa wewe ni mnyonge na kefule tu asiye na matumaini yo yote wala kesho yenye utukufu
Asubuhi ya leo nakuomba usimame wima na kuukana uwongo huu ulioshindiliwa ndani mwako kwa muda mrefu na mifumo gandamizi ya kijamii kiasi cha kukuondolea mng'aro wako na kukugeuza kuwa mpapasi tu asiyejua aendako.
Haupo hapa duniani kwa bahati mbaya na ukichunguza vizuri utaliona lengo na kusudio lako lililokufanya uje hapa duniani. Maisha yako yana maana na thamani sawasawa na ya binadamu mwingine ye yote - awe tajiri kupindukia, msomi aliyebobea, mtu mwenye umashuhuri wa kuandamwa kila aendako.....
Nyanyua shingo yako kama afanyavyo twiga - yule mnyama mlimbwende mpole na mwenye madaha. Jitahidi uone mbali zaidi kuliko wengine. Kaitazame dunia kwa jicho jipya. Nenda ukapambane !!!
Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) at Tuesday, June 12, 2012
Share
Mija Shija SayiJune 12, 2012 at 8:20 AM
Yaani wamarekani wako mbali sana katika maneno ya kutia moyo...
Kaka Matondo nashukuru sana kwa kipengele hiki maana mimi ni mdhaifu sana wa waneno yakutia moyo, yaani nayapenda sana.
Baraka kwako na familia.
Reply
Replies
Masangu Matondo Nzuzullima (MMN)June 12, 2012 at 7:25 PM
Da Mija;
Nimejifunza kuhusu kuanza kila siku kwa mtazamo chanya. Japo njia ya kawaida ni kutumia mafungu ya Biblia pamoja na maombi, hata maneno ya kawaida tu kama haya yanaweza kuwa na athari nzuri.
Basi pita hapa kila asubuhi kuyapata maneno haya ya kutia moyo.
Salami kwako pia, Manjula na familia yote. Mbarikiwe !!!
Reply
Yasinta NgonyaniJune 12, 2012 at 11:01 AM
Kaka Matondo ahsante kwa kutushirikisha katika maneno haya kwani nadhani tunahitaji kukumbushana na kutiana moyo. Nimeyapenda. Aamani Daima.
Reply
Replies
Masangu Matondo Nzuzullima (MMN)June 12, 2012 at 7:33 PM
Asante Da Yasinta...
Dunia hii inachosha na ni rahisi sana kukata tamaa. Kumbe tungejua watu wengine wanapambana na shida kubwa zaidi kuliko zetu, tungejikakamua na kushukuru hata kwa kuweza tu kuamka leo asubuhi tukiwa wazima na salama.
Kutiana moyo - hata kwa njia hii tu inaweza kutukumbusha kuyatazama mambo katika uzuri wake na siyo kulalamikia ubaya tu utafikiri kwamba ubaya na matatizo vimejitenga na mfumo mzima wa mambo.
Reply
AnonymousJune 18, 2012 at 12:07 PM
Asante kaka Matondo kwa hili. Nimepita hapa uani kwako baada ya muda mreeeeefuuu. Na leo , nimeamka nikiwa nimedorora vibaya sana kwa mawazo lukuki na kila siku kujihesabia mikosi na bahati mbaya.
Nadhani umetumika kunitia moyo maana nilikuwa napiga mwayo hadi ukaishia nusu. Najihisi tofauti ghafla na maneno ni ya kawaida sana lakini yamekuja kwa wakati!
Saingine tunasahau kuhesabu baraka ( Kwizukwa mbango).
Asante for this
Kipapli
Reply
Replies
Masangu Matondo Nzuzullima (MMN)July 16, 2012 at 8:06 AM
Asante ndugu yangu. Ni rahisi sana kujikita katika uhasi na kusahau mema na mibaraka tuliyonayo. Kumbe hata ile kuweza kuamka tu kitandani ni mibaraka tosha.
Tuendelee kutiana moyo ili tuweze kusonga mbele na safari yetu.
Mungu Aendelee kukubariki wewe na familia yako. Ikalagi mhola badugu bane !!!
AnonymousApril 4, 2013 at 12:09 PM
Prof.Dickison Kamgisha tuwasiliane kwa no.+0743592888, Kamgisha(x-Shidusa Chairman)
Reply
Links to this post
Create a Link
‹
›
Home
View web version
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni