Beki wa Liverpool ya Uingereza ahudhuria mechi ya kumuaga Ninja wa Yanga
KAMGISHA BLOG / 27 min
Mamadou Sakho (wa tatu kulia waliosimama) akiwa na kikosi cha Taifa Jang'ombe jana
BEKI wa kimataifa wa Ufaransa, Mamadou Sakho anayechezea Liverpool ya England usiku wa jana alikuwa mgeni maalum wakati wa mechi mahsusi ya klabu ya Taifa Jang’ombe kumuaga beki wake, Abdallah Hajji ‘Ninja’ anayehamia Yanga.
Ninja aliyesaini mkataba wa miaka miwili mapema mwezi huu kujiunga na Yanga, alicheza kwa dakika 10 tu baada ya kuingia kutokea benchi dakika ya 46 na Taifa Jang’ombe ikachapwa 2-1 na Mlandege.
Na Sakho alikuwepo uwanjani kama mgeni maalum akasalimiana na wachezaji wote, akapiga picha na vikosi vyote kabla ya kwenda jukwaani kushuhudia mchezo huo, mabao ya Mlandege yakifungwa na Abdallah Edi Mundo dakika ya 60 na Razak Khalfan dakika ya 78, wakati la Taifa lilifungwa na Ali Badru dakika ya 30.
Kabla ya hapo, Sakho alizuru kwenye kituo cha watoto yatima cha SOS Village ambacho kinaazimisha miaka 26 tangu kianzishwe na kutoa misaada mbalimbali.
Sakho yuko Zanzibar tangu Juni 17 baada ya kuwasili akitokea Ufaransa na anatarajiwa kuondoka kesho kurejea nyumbani, kuanza maandalizi ya msimu mpya baada ya mapumziko.
Kabla ya hapo, Sakho alikuwa pia Tanzania Bara kwa wiki moja na akazuru hadi mbuga za wanyama. Vyanzo vya uhakika vinasema, alirejea Ufaransa kabla ya kwenda Zanzibar.
Mchezaji huyo ambaye msimu uliopita alicheza kwa mkopo Crystal Palace, alizaliwa Februari 13, mwaka 1990 na kisoka aliibukia Paris FC kabla ya kuhamia timu ya vijana ya Paris Saint-Germain mwaka 2002 na Oktoba mwaka 2007 aliweka rekodi ya mchezaji kijana daima kuiongoza timu hiyo kam Nahodha katika Ligue 1.
Sakho amecheza mechi zaidi ya 200 katika klabu hiyo, akishinda nayo mataji yote manne ya nyumbani kabla ya mwaka 2013 kuuzwa Liverpool kwa dau la Pauni Milioni 18.
Mwaka huu alitolewa kwa mkopo Crystal Palace pia ya Ligi Kuu England ambako amekwenda kucheza mechi nane.
Sakho ni mchezaji wa kikosi cha kwanza cha wakubwa cha Ufaransa, ambaye awali amechezea timu zote za vijana na za nchi hiyo.
Tangu acheze mechi yake ya kwanza kikosi cha wakubwa cha Ufaransa mwaka 2010 dhidi ya England, Sakho amecheza mechi zaidi ya 25 na alikuwemo kwenye kikosi cha timu hiyo kwenye Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 nchini Brazil.
Mamadou Sakho (wa sita kulia) akiwa na kikosi cha Mlendege jana usiku wa Amaan, Zanzibar
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni