Tafuta katika Blogu Hii

Jumanne, 3 Januari 2017

Tatizo la Ugumba kwa wanawake

Tatizo la Ugumba kwa wanawake
Kamgisha blog / 6 hours ago

Ugumba ni hali ya mwanamke kushindwa kushika ujauzito. Linaweza kuwa tatizo pia kwa mwanaume lakini katika makala hii tutaona nini kinasababisha tatizo hili kwa upande wa wanawake.

Nini husababisha ugumba kwa wanawake?

Mayai kutokomaa ipasavyo:
Tatizo la mayai kutokukomaa vema ndilo chanzo na sababu kuu ya wanawake wengi kushindwa kushika ujauzito na hii inachukua karibu asilimia 30 ya wanawake wote wagumba. Habari njema ni kuwa tatizo hili linaweza kurekebishwa kirahisi ikiwa mwili utapewa vile viinilishe mhimu vinavyokosekana hadi kupelekea mayai kutokomaa vizuri.

Vinavyosababisha mayai ya mwanamke kutokomaa vema:

(1) Matatizo ya kihomoni
Matatizo katika homoni ndicho chanzo kikuu cha mayai kutunga bila kukomaa vizuri. Hatua za ukomaaji wa mayai zinategemea uwiano mzuri wa homoni na namna zinavyotegemeana katika kufanya kazi. Jambo lolote linalovuruga homoni kubaki katika uwiano wake sawa na wa kutegemeana na wenye kufanya kazi ipasavyo linaweza kupelekea utungaji wa mayai ambayo hayajakomaa vizuri. Kuna sababu kuu mbili zinazosababisha matatizo katika homoni:

Ufanyaji kazi usioridhisha wa hypothalamus
Hypothalamus ni sehemu ya mbele ya ubongo ambayo ina jukumu la kutuma ishara (signals) kwenda katika tezi ya pituitari ambayo yenyewe tena hutuma uchochezi wa kihomoni kwenda kwenye ovari katika mfumo wa F.S.H na L.H ili kuanzisha ukomaaji wa mayai. Ikiwa hypothalamus inashindwa kufanya kazi zake vizuri kutungwa kwa mayai ambayo hayajakomaa ndiyo kutakuwa ni matokeo yake. Tatizo hili linachukuwa asilimia 20 katika kesi za mayai kushindwa kukomaa kiasi kinachohitajika.

Ufanyaji kazi usioridhisha wa tezi ya pituitari
Kazi kubwa ya tezi ya pituitari ni kuzarisha na kutoa homoni mbili maalumu kwa ajili ya mfumo wa uzarishaji kufanya kazi zake vizuri ambazo zinajulikana kitaalamu kama ‘Follicle-stimulating hormone (F.S.H)’ na ‘Luteinizing hormone (L.H)’.  Mayai yatashindwa kukomaa vizuri ikiwa ama L.H au F.S.H zinatengenezwa chache sana au nyingi sana kuliko inavyohitajika. Hili linaweza kutokea kama sababu ya ajari, uvimbe au kama usawa usio sawa wa kikemikali katika pituitari.

(2) Kovu katika Ovari
Uharibifu au ajari katika ovari unaweza kupelekea kuzalishwa kwa mayai ambayo hayajakomaa. Kwa mfano, upasuaji mkubwa, uvamizi au upasuaji wa mara nyingi wa uvimbe katika ovari unaweza kusababisha kapsuli ya ovari kupata majeraha au makovu na hivyo kwa namna moja ama nyingine kuweza kuzuia utungwaji wa mayai ambayo hayajakomaa vema. Pia maambukizi katika njia ya uzazi yanaweza kupelekea tatizo hili.

(3) Dalili za mwanzo za kukaribia kufunga kuzaa (Menopause)
Hii huchangia kwa asilimia chache na kwa sasa halielezeki kisawasawa. Kwamba wanawake wengi wanapokaribia umri wa kuacha kuzaa kuanzia miaka 40 kwenda juu baadhi yao hutokewa na tatizo la kutunga mayai ambayo hayajakomaa vema. Baadhi ya wanawake wanaacha kupata siku zao mapema kabla ya umri uliozoeleka yaani miaka 40 kwenda juu.

Kwa sababu hiyo inadhaniwa kwamba uwezo wao wa asili katika kuzalisha mayai unakuwa umepunguwa na wengi wao huwa ni wale walikuwa wakijihusisha zaidi na michezo ya kukimbia au wale wenye historia ya muda mrefu ya kuwa na uzito pungufu na wafanyaji sana wa mazoezi. Tatizo hili pia linaweza kuwa ni la kurithi.

(4) Matatizo kwenye kijishimo yai (follicle) katika ovari:
Ingawa kwa sasa bado hili nalo halielezeki, hiki kijishimo yai kwa kitaalamu kinajulikana kama ‘’follicle’’ ndicho hupasuka na yai kutoka. Kuna baadhi ya kina mama wanapata dalili za kijishimo yai kutokupasuka “unruptured follicle syndrome” na matokeo yake kila mwezi mama anazalisha yai kama kawaida lakini hiki kijishimo yai kinashindwa kupasuka. Hivyo yai linabaki ndani ya ovari na utungaji wa mimba unashindwa kufanyika.

Kinachosababisha ufanyaji kazi dhaifu wa mirija ya uzazi (Fallopian Tubes):

Magonjwa katika mirija ya uzazi yanahusika na ugumba kwa karibu ya asilimia 25 ya wanawake wote wagumba. Hali yenyewe inatofautiana toka kwa mmoja hadi kwa mwingine kutoka kugandana au kunatana kidogo hadi kuzibika kabisa kwa mirija. Matibabu ya mirija iliyozibika huhusisha upasuaji au usafishaji wa mwili kwa kula vyakula na vinywaji maalum kwa muda wa majuma kadhaa.

Sababu kubwa zinazopelekea kuzibika au kunatana kwa mirija ya uzazi ni pamoja na zifuatazo:

(A) Maaambukizi
Maambukizi katika njia ya uzazi ambayo yamesababishwa ama na bakteria au virusi na ambayo kwa kawaida ni magonjwa ya kuambukizana kwa njia ya tendo la ndoa, maambukizi haya kwa kawaida husababisha muwasho au kuungua na kupelekea makovu na uharibifu. Magonjwa ya zinaa kama vile kisonono na mengineyo yanaweza kuwa chanzo cha ugumba kwa wanawake wengi hasa ikiwa hayatatibiwa mapema.

(B) Magonjwa yasiyo ya kawaida
Magonjwa yasiyo ya kawaida ni pamoja na ugonjwa wa kidole tumbo (appendicitis) na uvimbe katika utumbo mpana (colitis), magonjwa ambayo husababisha muwasho au kuungua chini ya uvungu wa utumbo mkubwa na kuiathiri mirija ya falopiani na kama matokeo yake makovu na kuzibika kwa mirija ya uzazi hutokea.

(C) Upasuaji uliopita
Upasuaji una chukua nafasi kubwa katika kusababisha ugumba kutokana na matokeo yake ya kusababisha magonjwa ya mirija ya uzazi na uharibifu utokanao na huo upasuaji. Upasuaji katika utumbo mkubwa unaweza kupelekea kunatana au kugandana kwa mirija ya uzazi kutakakopelekea mayai kushindwa kusafiri kirahisi katika mirija hiyo ya uzazi.

(D) Mimba kutungwa nje ya mji wa uzazi:
Hii ni wakati mimba inapotungwa katikati ya mirija ya uzazi yenyewe. Katika hali kama hii hata kama kutatokea bahati kiasi gani bado kunaweza kusababisha uharibifu katika mirija na hali hii ni moja ya hali mbaya sana kiafya na kimaisha.

(E) Hali ya kurithi
Kwa nadra au kwa asilimia fulani ndogo baadhi ya wanawake huzaliwa na hali ya kuwa na mirija isiyo ya kawaida kwa uzazi na kwa kawaida hali hii huambatana na mji wa uzazi usio wa kawaida pia. .

(5)  Sababu za kitabia:
Inajulikana wazi kwamba baadhi ya tabia na namna tunavyoishi kunaweza kupelekea wanandoa wakashindwa kupata mtoto. Kwa bahati nzuri nyingi kama si zote ya hizo tabia zinaweza kurekebishika au kuachwa kabisa na kupelekea siyo tu kuwa na uwezo wa kuzaa bali pia kuwa na afya nzuri kwa ujumla. Sababu hizo za kitabia ni pamoja na zifuatazo:

Lishe na mazoezi
Ili mfumo wa uzazi uwe na uwezo mzuri unahitaji vitu viwili mhimu, lishe kamili na mazoezi. Wanawake wenye uzito uliozidi sana au wenye uzito pungufu sana wanaweza wakapatwa na tatizo la kutopata ujauzito kirahisi.

Uvutaji sigara
Uvutaji wa sigara una mchango mkubwa na ugumba. Uvutaji sigara husababisha uzarishwaji wa mbegu chache kwa mwanaume (lower sperm count) kwamba mwanaume anatoa mbegu chache sana ama pungufu wakati huo huo uvutaji sigara huchangia katika tatizo la kutoka kwa mimba, kuzaa kabla ya miezi 9 (njiti), na kuzaa mtoto mwenye uzito mdogo kwa wanawake.

Unywaji pombe
Unywaji pombe kupita kiasi una mchango mkubwa sana katika ugumba na hii hata ikitokea mama akapata ujauzito kama bado anaendelea kunywa pombe inaweza kupelekea matatizo hata kwa mtoto mtarajiwa. Unywaji pombe pia huchangia uzarishwaji wa mbegu chache kwa wanaume.

Madawa ya kulevya
Utumiaji a madawa ya kulevya kama bangi na mengine ya kujidunga kwa sindano kunaweza kuwa sababu ya kuzalisha mbegu chache kwa wanaume. Utumiaji wa dawa za kulevya kama ‘Cocaine’ kwa mama mjamzito kunaweza kusababisha mtindio wa ubongo na matatizo katika figo kwa mtoto mtarajiwa. Matumizi ya madawa ya kulevya inafaa yaepukwe wakati wa kutafuta ujauzito na wakati wa ujauzito.

Utowaji mimba
Utowaji mimba wa mara kwa mara pia unahusika sana na tatizo la ugumba kwa karibu ya asilimia 20. Utowaji mimba unaweza kusababisha makovu katika mji wa uzazi na hata kuharibika kabisa kwa mji wa uzazi ikiwa utowaji huo haukufanyika kitaalamu au unafanyika mara kwa mara.

(6) Sababu za ugumba za kimazingira:
Uwezo wa kushika ujauzito unaweza pia kuathiriwa kutokana na kuwa karibu na baadhi ya kemikali au sumu katika maeneo ya kazi au makazi. Vitu viwezavyo kusababisha mabadiliko, dosari za kuzaliwa, utokaji mimba, au utasa huitwa ‘Sumu kwa mfumo wa uzazi’. Kamikali zifuatazo zinahusishwa na ugumba au utasa:

Risasi (Lead)
Kuwa karibu na kemikali au sumu zinazounda risasi kunaweza kuwa sababu ya ugumba. Risasi hupelekea kuzalishwa kwa mbegu zisizo za kawaida kwa wanaume zijulikanazo kwa kitaalamu kama ‘teratospermias’ na inafikirika pia kuhusika na utokaji mimba kusiko kwa asili (artificial abortion).

Baadhi ya matibabu na madawa ya hospitalini
Kuwekwa kwenye matibabu yanayohusisha mionzi (x-rays), mionzi ya kawaida au hata ile ya kutibia kansa (chemotherapy), kunaweza kusababisha matatizo katika uzarishwaji wa mbegu kwa mwanaume na wakati huo huo kuchangia kwa sababu kadhaa zinazopelekea kutungwa kwa mayai ambayo hayajakomaa vizuri. Pia matumizi ya dawa za kuzuia ujauzito kwa muda mrefu yamekuwa yakihusishwa na ugumba kwa miaka ya hivi karibuni ingawa bado kuna mjadala mkubwa katika hili.

Ethylene Oxide
Hii ni kemikali inayotumika kusafishia vifaa vya upasuaji, pia hutumika katika kutengeneza baadhi ya sumu za kuua wadudu. Ethylene oxide inaweza kupelekea matatizo katika uzazi hasa katika miezi ya mwanzo mwanzo ya ujauzito na inahusishwa sana na tatizo la utokaji mimba katika miezi ya mwanzo ya ujauzito (early miscarriage).

Dibromochloropropane (DBCP)
Hii pia ni kemikali au dawa inayotumika katika kuua wadudu, ikiwa unafanya nayo kazi kila mara inaweza kusababisha kutungwa kwa mayai yasiyokomaa vizuri, kuelekea mapema kwa ukomo wa kutokuzaa kabla hata ya miaka 40 au 45 (early menopause) na kadharika.

(7) Sababu zingine zinazoweza kusababisha ugumba kwa mwanamke:
Karibu asilimia 10 ya ugumba kwa wanawake ni matokeo ya mji wa uzazi usio wa kawaida (abnormal uterus).  Hali zingine ni pamoja na uvimbe katika kizazi, kugandana au kunatana kwa mji wa uzazi na mirija ya uzazi.

Karibu asilimia 3 ya ugumba kwa wanawake ni matokeo ya matatizo ya ute usio wa kawaida katika mlango wa kizazi (femaleís cervical mucus). Ute ute huu unahitaji kuwa na hali fulani maalumu kwa mbegu za kiume kuweza kuogelea kirahisi katikati yake. Chanzo kikubwa cha tatizo hili ni usawa usio sawa wa homoni za kike ambapo homoni ya uzazi ya kike iitwayo ‘estrogen’ yaweza kuwa ni chache sana au homoni nyingine iitwayo ‘progesterone’ yaweza kuwa ni nyingi sana tofauti na inavyohitajika.

Vitu vya kuepuka kwa mtu mwenye tatizo la ugumba:

Chipsi
Vinywaji baridi
Kaffeina
Nyama nyekundu
Vilevi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni