Tafuta katika Blogu Hii

Jumamosi, 16 Desemba 2017

NINGEMSIKILIZA

Mimi na yeye tulikuwa na harusi nzuri. Tulitegemea ndoa yetu itadumu kwa muda mrefu. Tulikuwa na ndoto na mipango mikubwa. Oh tulikuwa na mawazo makubwa mpaka pale nilipopotea njia...


Mungu alinibariki, yes alinibariki sana. Mke mzuri mikononi mwangu ambae kila mwanaume angetamani kuwa nae. Watoto wazuri watatu wenye afya na kazi iliyokua ikinilipa vizuri.


Nilikuwa nalipwa mshahara mzuri, hivyo nikafikiri namna ya kuufurahia zaidi. Taaratibu nikaanza kujisogeza club na pubs mbalimbali nikinywa hata bia moja.


Bia moja zikawa mbili, zikawa tatu...pombe akawa rafiki yangu mpya. Kuniona kwenye Bar ikawa kama dini yangu. Nilikuwa na pesa hivyo pombe ilitakiwa iniabudu.


"Mhudumu, wazungushie wale wote" nilikuwa nikipiga kelele za kilevi kila nilipokuwa Bar. Walevi wakaanza kunifurahia...nikawa celebrity Bar zote hot zilizopo mjini, kuanzia Sewa Bar, Catalunya, hata Corner Bar...


Lakini nyumbani nilikuwa mbogo, mke wangu akawa akiniuliza nakuwa mtu wa aina gani? Alikuwa akilia..akinililia jinsi nilivyobadilika...
.
Mke wangu alikuwa akinililia niwahi kurudi nyumbani, lakini sikuwa namsikia. Unajua nini? Nilikuwa nawaza kuwa nimeshamuoa kwaiyo haina haja ya kum-please!


Nilikuwa naona kama ananiwekea kiwingu tu, wanawake wa Bar walikuwa wakinipenda. Mke wangu aliniona nimekuwa kama mtoto mdogo na mimi niliona mke wangu anajiona kama mama yangu kunizuia starehe zangu..!


"Unaanzaje kumruhusu mwanamke akwambie nini cha kufanya? Nani kichwa cha nyumba? Mzibe mdomo wake.." Marafiki zangu wa Bar walinishauri hivyo.


Niliwasikiliza washikaji wangu kwa sababu walikiwa wakinifanya nijione kama mfalme, wakati nyumbani nilikuwa nashindwa kutimiza majukumu kama mfalme kwa malikia mke wangu.


Nilikuwa mume na baba niliefeli kwenye majukumu yangu. Nilichokua najua ni kupiga makelele Bar kama mbwa na kufukuzia wanawake wa Corner Bar na kwingineko waliojikatia tamaa.


Usiku baada ya usiku silali nyumbani. Mke wangu akaanza kukata tamaa..akaacha kunitafuta..mke mwenye heshima zake humtafuta mfalme wake aliko, sio mbwa apigae kelele kwenye Bar..akaanza kujifunza kuishi bila mimi.


Alichoka kuniambia kwamba napoteza pesa, pesa zetu, naharibu ndoa yetu, naharibu nyumba yetu..wale wanawake waliojikatia tamaa wakawa waki-sex na mimi na kunila pesa zangu huku wengine wakiniibia pale napolewa.


Washikaji zangu nao wakawa wakinitumia mimi kama mgodi wa pesa kujihudumia mahitaji wanayotaka..nilikuwa nahitaji kuabudiwa na kunyeynyekewa..pedeshee mtoto!!


Lakini nyumbani nilikuwa mbahili, zaidi ya milioni 50 zilinipotea kwa mambo ya kipuuzi. Niliwapa faida kiwanda cha Bia, lakini hata kuwanunulia nguo wanangu nilishindwa.


Nilipewa onyo za kutosha ofisini kwa sababu ya kwenda kazini huku nimelewa, nikawa nafanya kazi chini ya kiwango..mara tatu nimesababisha ajali..kwa kuendesha huku nikiwa nimelewa..


Wala sikutilia maanani kuonywa na wakubwa wangu wa kazi, kama nilivyokua simtilii maanani mke wangu..


Mtu yeyote aliekuwa anakuja kwa nia ya kunitenganisha na pombe akawa ni adui yangu mkubwa..nikawa na maadui wengi..


Mke wangu akiwa adui yangu namba moja. Mke wangu, mama wa watoto wangu..mwanamke niliyemuoa naishia kumpa stress na kupoteza uzuri wake waote..alishindwa kuvumilia zaidi...pale nilipoanza kuja na malaya ndani ya nyumba yetu...tena mbele ya watoto...


Akabeba mabegi yake, akachukua watoto wetu na kuondoka na kuniacha...


Nikafukuzwa kazi, nikanyang'anywa nyumba ya kampuni, nikanyang'anywa gari na mali zote za kampuni....


Nikapoteza marafiki, nikapoteza hata wale wanawake waliokuwa wakinipa sex..nikapoteza na heshima yangu..na ndoto zangu zote..lawama ni kwa pombe!


Lakini hapana, lawama si kwa pombe, najilaumu mwenyewe, najilaumu kwa msimamo wangu wa kipuuzi na najilaumu kutomsikiliza mke wangu na kuwa upande wa marafiki feki ambao wapo unapokuwa na pesa tu.


Sasa hivi niko hapa kitaa, Bar ya mtaani tu, nimepanga chumba kimoja kisichokua na umeme na nadaiwa kodi ya miezi mitatu..niko nimelewa, pombe za kienyeji nikiimba nyimbo za dini kujifariji..


Bado nashangaa nitapata wapi pesa ya kodi, nitapata wapi pesa ya matibabu kutibu madhara ya pombe kali iliyoharibu INI langu.


Niko hapa, mikono yangu inatetemeka.
Nimeshika glass ya pombe ya kienyeji.
Pombe imekua ndio kila kitu kwangu japo ya maladhi niliyonayo.


Ghafla namuona mke wangu anaonekana kwenye TV iliyopo kwenye kilabu cha mama Muuza. Anafanyiwa interview..Kampuni yake ya vipodozi inafanya vizuri..


Anaongelea biashara, GDP ya nchi na ajira kwa vijana na wanawake..


Na mimi niko hapa kwa mama muuza, sina hata mia..pombe ya kienyeji nimekopa....


"Mama muuza eeh ongeza sauti ya tv..!!" Napiga kelele kwa muuzaji.


Mke wangu yuko mbali, wote tungekua mbali kama ningemsikiliza...


"Aah mama muuza kama vipi zima TV, au badilisha channel.." Naropoka kilevi!
___________________________


Wanaume, tujifunze kusikiliza wake zetu. Wameumbwa kwa ajili ya kutusaidia..tuache watusaidie..wao pekee ndio wenye best interest na sisi kwenye mioyo yao...


Toa Maoni yako hapa chini:


Njia 10 Za Kupunguza Magonjwa Ya Mlipuko Wa Kuku

Njia 10 Za Kupunguza Magonjwa Ya Mlipuko Wa Kumgisha Blog · 8 hours ago




Mlipuko wa magonjwa ni moja ya sababu za hasara kubwa kwa wafugaji na vifo vinavyotokea kwa wakati mmoja. Pindi mfugaji anapokumbwa na janga la vifo vya ndege, kabla ya kufikia mwisho wa mzunguko wa uzalishaji hivyo basi asitarajie kupata faida nzuri mara baada ya mauzo. 
Hasara itokanayo na vifo inaweza kuepukika au kupunguzwa na kutokea kwa kiasi kidogo. 

Hili linawezekana, ifuatayo ni namna ya kufanikisha hilo;- 

1. Osha vyombo vya maji kila wakati na mwaga maji yaliyobaki. 
Hakikisha unamwaga maji yaliyosalia mbali na kuosha chombo na sabuni kila siku, weka maji safi yasiyo na dawa na wala usitumie maji ya mto au yale usiyoyajua chanzo chake. Kama utaweka maji dawa basi tumia ‘vitamini’ muhimu kama ‘vitalyte’ ambazo zinasaidia kuua vijidudu. 

2. Wape maji kabla ya chakula. 
Ndege wapo tofauti na binadamu au wanyama wengine. Hakikisha unawapa maji kabla ya chakula hasa kama unatumia maranda, hii ni kuhakikisha hawakanyagani wanapogombania chakula sehemu moja. 

3. Usiwape chakula chenye uvundo. 
Ni hatari sana kuwapa ndege/kuku wako chakula chenye ukungu, ni kama kuwalisha sumu. Ukungu au uvundo huwafanya kuku waugue kirahisi sana au kuwasababishia madhara mengine kiafya. 

4. Fuatilia kwa makini ratiba za chanjo na tiba. 
Mfugaji unatakiwa kupata tiba na chanjo sahihi kwa ndege unaowafuga. Kuchanja ndege kutasaidia sana kuimarisha kinga yao dhidi ya magonjwa hatari kama kideri, ndui, gumboro na mareksi. Dawa kama vile za minyoo na antibayotiki ni muhimu sana kwenye afya ya kuku na ndege wengine. 

5. Nunua na fuga vifaranga wenye afya njema. 
Matatizo mengi ya afya ya ndege au kuku ni matokeo  ya maisha duni ya awali ya kuku hao au huwa wanarithi. Itambulike hivi, baadhi ya ndege/kuku hurithi afya mbovu kutoka kwa wazazi wao. Hata hivyo baadhi ya watotoleshaji pia wanafuga kuku ambao wana afya mbovu na hivyo huuza vifaranga au mayai dhaifu na waathirika na hivyo mnunuzi anajikuta ananunua matatizo. 

6. Zuia mkusanyiko wa hewa ya ammonia. 
Maranda yakikaa muda mrefu bandani, hufanya hewa ya ammonia kuzalishwa kwa wingi, hewa hii hufanya ndege wapaliwe hadi kufa. Kila mara ondoa maranda mabichi au yaliyovunda na weka mengine haraka iwezekanavyo ili kuepuka vifo vitokanavyo na kupaliwa au magonjwa ya mfumo wa hewa. 

7. Zuia panya na vicheche. 
Banda la ndege linatakiwa lisiruhusu panya au wanyama wadogo jamii ya kicheche kuingia ndani, na ndege wa mwituni kwa kuweka nyavu au kupulizia dawa, ikiwa watapata upenyo wataua na kula ndege/kuku wako na kuacha vimelea vya magonjwa wanapokula vyakula au kunywa maji ya ndege wako. 

8. Zingatia usafi na usalama. 
Kipengele hiki cha usafi na usalama ni kipana  ila unachotakiwa kufanya ni kuzingatia usafi nje na ndani ya banda. Unatakiwa ukamilishe usalama wa afya ya ndege/kuku wako kila wakati, jambo ambalo wafugaji wengi hutekeleza pindi wanapo shitukizwa na mlipuko wa magonjwa. 

9. Wape chakula cha kutosha. 
Ndege kama walivyo wanyama wengine, hawawezi kukua na kuzalisha vizuri endapo wanapewa chakula duni na kidogo. Chakula bora ni msingi imara  na ni kinga kwani chakula duni hupelekea uzito kupungua na kinga kuwa chini na hivyo hufa mapema. Jitahidi wape kuku chakula cha kutosha ila usiwazidishie. 

10. Wakinge dhidi ya baridi kali. 
Baridi kali ni adui kwa afya ya wanyama, ndege na binadamu. Jaribu kila uwezavyo kuwakinga kuwakinga ndege wako na baridi kali kwani inaua haraka sana kama sumu. Wawekee chanzo cha joto wakati wa baridi au jenga banda ambalo halipitishi baridi kali. 

Hizo ndizo njia muhimu ambazo ukiwa mfagaji unazoweza kuzitumia ili kukinga magonjwa yanatokanayo na kuku.

Kama Unaogopa Kufanya Kitu Hiki, Sahau Kuhusu Mafanikio Katika Maisha Yako Yote

Kama Unaogopa Kufanya Kitu Hiki, Sahau Kuhusu Mafanikio Katika Maisha Yako Yote

Kamgisha Blog · 5 hours ago



Fikiria kila unachokijua na kukikumbuka kuhusu mabadiliko unayotaka yawe katika maisha yako, halafu  uone ukweli huu  kama kweli nawe ni mmoja kati ya watu wanaotaka mafanikio au uko nje ya mstari wa mafanikio na pengine tu wewe hujijui. Kama kweli unataka mafanikio, ni kwanini  mara kwa mara umekuwa ukisita au kuogopa kufanya jambo ambalo lingeweza kubadili maisha yako na kukuletea mafanikio mkubwa? Hili ndilo tatizo walilonalo watu wengi wanahofia sana kufanya mabadiliko kwa namna moja au nyingine hata kwenye yale malengo waliojiwekea wao wenyewe kuna wakati huwa wanaogopa pia. 

Kimaumbile, kila binadamiu anahofia mabadiliko, lakini hofu ya mabadiliko inapozidi kuwa kubwa na kukuzuia kufanya mambo ya maana kwako, hofu hii  sasa hugeuka kuwa ni maradhi yanayokuzuia wewe kufanikiwa. Hebu fikiria tena, ni mara ngapi umekuwa ukitaka kufanya mabadiliko Fulani  katika maisha yako, lakini umekuwa ukijikuta ukishindwa kufanya hivyo kutokana na kuogopa kufanya vitu Fulani? Ni mara ngapi umekuwa ukitaka kuingia kwenye biashara lakini umekuwa na hofu nyingi zinakuzuia? Hivi ndivyo ilivyo mabadiliko huogopwa, wakati mwingine bila sababu ya msingi. 

Wengi wetu kutokana na kuogopa mabadiliko, hujikuta ni watu wa kutoa sababu ambazo hata hazina mashiko zinazosababisha wao washindwe kutekeleza malengo na mipango waliojiwekea. Utakuta mtu anakwambia  hawezi kufanya biashara ni kwa sababu hana mtaji, ukija kuchunguza kidogo utagundua kuwa hiyo ni sababu ambayo amekuwa akiitoa kwa muda mrefu, iweje kila siku mtu huyohuyo awe hana mtaji tu. Kama uko hivi una hofu tu hata kwa vitu vidogo ambavyo ungeweza kuvifanyana , tambua kuwa kuanzia sasa unaye adui mkubwa ndani mwako anayekuzuia kufanikiwa. Na unapoogopa kufanya mabadiliko ambayo unaahitaji sasa ili ufanikiwe, sahau kuhusu mafanikio katika maisha yako yote. 

Tatizo kubwa utakalokuwa nalo linalosababishwa na hofu hii ya kuogopa kufanya mabadiliko ni lazima utakuwa mtu wa kutaka mafanikio ya harakaharaka. Watu wengi wenye mawazo ya kutaka kufanikiwa leoleo hata kama wameanza biashara leo, wengi wao huwa wana hofu hii kubwa ya mabadiliko ndani mwao, unaweza  kufanya utafiti mdogo utagundua ukweli huu ulio wazi. Hawa ni watu ambao kiuhalisia hawaijui wala kuiamini subira ndani mwao, bali ni watu wakutaka mfumo wa maisha uwe ambao unaanza leo biashara na wiki ijayo uwe tajiri ni kitu ambacho hakiwezekani kabisa. 

Hivi ndivyo walivyo watanzania wengi wanaogopa mabadiliko na kuamini katika miujiza, sio katika wao wenyewe kutenda na kuona matokeo.  Hebu jaribu kukagua maisha ya walio wengi utakuja kugundua ukweli huu ni watu wanaofikiria sana leo, sasa hivi, siyo baadaye. Hata malengo yao ni ya karibu sana na hawataki shida, wanataka wafanye leo, wamudu leo na kila kitu kimalizike leo. Sijui kesho watafanya kitu gani? Ukimwambia mtanzania aanzishe mradi ili aje faidi baada ya miaka 10 kutoka sasa kwanza atakushangaa, kisha atakucheka we hadi mbavu zimuume. Anataka leo hata kama ni kwa miujiza. 

Ndiyo maana wengi kati ya Watanzania hawana malengo, wanaishi tu na kutawaliwa na hofu za mabadiliko. Kuweka malengo siyo sehemu ya maisha yao, kwani malengo yanataka mtu mwenye subira, mtu anayeamini kwamba maisha ni kuanguka na kusimama. Wanachojua kikubwa ni kulalamika na kulaumu, kuponda na kukejeli, kwa sababu wao wamekata tamaa bila kujijua. Ndiyo maana ni watanzania wanne tu kati ya kumi ambao wanafanya kazi, wanatoka jasho na wanaweza kusubiri bila kukata tamaa, wengine waliobaki wanasubiri ujanja ujanja tu ilimradi wafanikiwe hata kama ni kwa kufanya uhalifu wa aina yoyote. 

Ni watu ambao wanataka kuishi kihadithi, wawe na pete ambayo wanaweza kuiamuru iwape wakitakacho na wakipate. Maisha ni ya kibunuasi- abunuasi tu, watu hawa kwao mabadiliko ni kitu kigumu sana kwao na kinaogopwa kweli. Kama unataka mafanikio ya kweli yawe kwako, unatakiwa kubadilisha fikra za zako na kuamua kukubali kuwa mafanikio yanahitaji mabadiliko makubwa sana ambayo wewe mwenyewe unatakiwa uyafanye kwa kujitoa hasa. Acha kuwa na hofu zisizo na maana zinazokuzuia wewe usifanikiwe, chukua hatua katika maisha yako, kuyafikia maisha unayoyataka.